Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI kimefanikisha mnada wake wa kwanza wa zao la korosho kwa msimu wa mwaka 2025, ambapo wakulima kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale wameuza jumla ya kilo 20,630,516 za korosho kwa bei ya juu ya shilingi 2,610 na ya chini shilingi 2,460 kwa kilo. Mauzo hayo yamefanyika kwa uwazi kupitia mfumo wa soko huru la mtandaoni unaoleta ushindani wa kweli.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Hassan Ngoma, amepongeza ufanikishaji wa mnada huo na kusisitiza kuwa mfumo wa soko la mtandaoni unatoa nafasi ya wakulima kunufaika na bei halisi ya soko. Ameitaka mamlaka husika kuhakikisha wakulima wanalipwa mapema ili waweze kutumia fedha zao kwa maandalizi ya msimu ujao.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika, Bi. Consolata Kiruma, amewashukuru wakulima kwa kushiriki kwa wingi na kuhimiza kuendelea kusimamia ubora wa korosho, hasa katika hatua ya ukaushaji, ili kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa. Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maadili, uaminifu na uadilifu katika usimamizi wa vyama vya ushirika.
Mkulima kutoka Ruangwa, Bi. Amina Njoro, amepongeza uendeshaji wa mnada huo akisema umeleta matumaini kwa wakulima na kuwa bei iliyopatikana imewaridhisha. Ameomba serikali kuendelea kuimarisha utendaji wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi kupitia mfumo wa mnada.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho (CBT), Bw. Francis Alfred, amewapongeza wakulima waliofanikisha mauzo hayo na kuwataka kuendelea kulinda ubora na thamani ya zao la korosho. Amesema ubora katika ukaushaji na uhifadhi ni msingi muhimu wa kuongeza tija na ushindani wa korosho za Tanzania katika soko la kimataifa.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.