Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mheshimiwa Goodluck Mlinga, amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kutanguliza masilahi ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yao. Ametoa kauli hiyo Disemba 4, 2025, wakati wa mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kutwa Liwale (Liwale Day).
Akizungumza katika mkutano huo, Mlinga amesisitiza umuhimu wa madiwani kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa halmashauri pamoja na watendaji wa serikali ili kuleta maendeleo kwa wananchi. Amesema juhudi na utendaji wao ndizo zitakazoamua mustakabali wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2030, akiwatahadharisha kuwa “watakachokipanda ndicho watakachokivuna.”
Katika kuimarisha uchumi wa vijana, Mlinga amewashauri madiwani kuwahamasisha kufungua vikundi na kuandaa maandiko mazuri yatakayowawezesha kupata mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, amewataka kupanga mikakati ya kuwapatia vijana maeneo ya ardhi angalau hekari 10 kila mmoja kwa ajili ya shughuli za kilimo na kuzuia uuzaji holela wa ardhi katika kata zao.
Katika sekta ya elimu na huduma za jamii, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka madiwani kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto shuleni ifikapo mwezi Januari. Pia amewataka kusimamia kukamilika kwa miradi ya maendeleo inayoendelea, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya na huduma za umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Aidha, katika masuala ya ufugaji, Mlinga amewataka madiwani kuhakikisha wafugaji wanatumia maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji ili kuepusha migogoro na matumizi mabaya ya ardhi. Alisisitiza kuwa utekelezaji wa maagizo hayo utachangia kuimarisha ustawi na maendeleo katika wilaya ya Liwale.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.