Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mheshimiwa Goodluck Mlinga, ameagiza viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na maghala makuu kuhakikisha utendaji kazi unafanyika kwa saa 24, usiku na mchana, ili kurahisisha upokeaji na usafirishaji wa korosho kutoka kwa wakulima. Amesema hatua hiyo inalenga kuondoa usumbufu wanaoupata wakulima wanapofikisha mazao yao katika maghala, hali ambayo imekuwa ikisababisha ucheleweshaji na msongamano mkubwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika ghala kuu la Chama cha Ushirika cha Msingi Umoja na ghala kuu la Hassan Yasin Mpako, Mheshimiwa Mlinga amesema utaratibu huo utasaidia kuongeza ufanisi katika mzunguko wa ukusanyaji na usafirishaji wa korosho. Ameeleza kuwa kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara na upungufu wa magari ya kusafirisha korosho, kufanya kazi kwa saa 24 kutayawezesha magari yaliyopo kufanya safari zaidi ya moja kwa siku.
Mlinga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika na watendaji wa maghala kuhakikisha mazao yanapokelewa kwa wakati na kwa utaratibu unaoendana na miongozo ya Bodi ya Korosho. Amesema uwajibikaji wa pamoja katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho utasaidia kuongeza tija kwa wakulima na kuimarisha soko la zao hilo.
Akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya (KUU), Mheshimiwa Mlinga alitumia ziara hiyo pia kujionea kiwango cha korosho kinachofikishwa na wakulima katika maghala hayo, na kuahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maagizo hayo.
Along Nachingwea Road opposite DDD Quarters
Sanduku la Posta: P.O. BOX 23 LIWALE
Simu ya Mezani: 023 2937043
Mawasiliano ya mkononi:
Baruapepe: ded@liwaledc.go.tz
Hakimiliki 2023 © Halmashauri ya Wilaya ya Liwale. Haki zote zimehifadhiwa.